SHERIA YA NDOA TANZANIA KUREKEBISHWA
Naibu Waziri wa Sheria
na Katiba, Angellah Kairuki amesema kuwa Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971
iko kwenye mchakato wa kurekebishwa kutokana na utata unaokinzana na
sheria nyingine za masuala ya kijinsia.
Akizungumza baada ya
ufunguzi wa warsha ya siku moja ya waandishi wa habari na sheria na sera
zinazohusu ukatili wa kijinsia iliyoandaliwa na Taasisi ya Champion na
Engender Health wilayani Bagamoyo juzi, Kairuki alikiri kuwepo kwa utata
wa sheria hiyo jambo linaloendelea ukatili hasa kwa wanawake.
“Utata wa sheria ya ndoa
ya mwaka 1971 ulijadiliwa katika Baraza la Mawaziri na walishafika
mbali. Lakini ilionekana kwa kuwa masuala ya ndoa na mirathi yanagusa
mila, desturi, dini na tamaduni za watu, ilionekana siyo rahisi kutunga
sheria haraka,” alisema Kairuki na kuongeza:
“Wapo wanaosema mtoto
hawezi kuolewa akiwa na miaka 14 na wapo wanaosema anaweza. Baraza la
Mawaziri liliamua kuwa kuwe na kura ya maoni (white paper).”
Hata hivyo alisema kuwa
wakati mchakato huo ukikaribia kuanza uliingiliana na mabadiliko ya
Katiba. Hivyo alisema kura hiyo ya maoni itafanyika baada ya kupatikana
kwa Katiba Mpya.
Awali akifungua warsha
hiyo, Kairuki alisema kuwa Serikali imechukua hatua za kukabiliana na
ukatili wa kijinsia ikiwa pamoja na kuanzisha dawati la jinsia na watoto
kupitia Jeshi la Polisi na timu za ulinzi na usalama wa watoto kupitia
Idara ya Ustawi wa Jamii.
Akitoa mada katika
warsha hiyo, Mkurugenzi Msaidizi wa Taasisi ya Engender Health, Dk
Monica Mhoja alisema Serikali ya Tanzania inasifika kwa kuridhia sheria
na mikataba ya kimataifa kuhusu ukatili wa kijinsia, lakini
hazitekelezwi ipasavyo.
“Tunapokuwa kwenye
majukwaa ya kimataifa, Tanzania tunasifika kwa kuridhia sheria na sera
nyingi, wanapotuhoji kuhusu utekelezaji inakuwa shida,” alisema Dk Mhoja.
0 maoni:
Chapisha Maoni