Jumamosi, 22 Machi 2014

HOTUBA YA JK,WAKATI WA KULIHUTUBIA BUNGE MAALUM LA KATIBA

Mheshimiwa Samuel Sitta, Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba;
Mheshimiwa Dkt. Mohamed Gharib Bilal, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi;
Mheshimiwa Mizengo Peter Pinda, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Maalim Seif Sharif Hamad, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar;
Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Mheshimiwa Anne Semamba Makinda; Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano;
Mheshimiwa Pandu Ameir Kificho, Spika wa Baraza la Wawakilishi na Mwenyekiti wa Muda wa Bunge Maalum la Katiba ;
Mheshimiwa Rashid Othman Chande, Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Othman Makungu, Jaji Mkuu wa Zanzibar;
Viongozi Wakuu Wastaafu;
Waheshimiwa Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba;
Waheshimiwa Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba;
Wageni waalikwa;
Mabibi na Mabwana;
Pongezi
Nakushukuru sana Mheshimiwa Mwenyekiti kwa kunipa fursa ya kuja kuzungumza na Waheshimiwa Wajumbe wa Bunge letu Maalum la Katiba katika siku hii muhimu na ya kihistoria kwa nchi yetu. Nimekuja kuwatakia heri na naungana na Watanzania wenzetu wote kuwaombea baraka za Mwenyezi Mungu, ili muweze kuifanya kazi yenu kwa utulivu, hekima, umakini mkubwa na kuimaliza kwa salama na kwa mafanikio yanayoyatarajiwa na Watanzania.
Natoa pongezi nyingi kwako na kwa Makamu wako kwa kuchaguliwa kwenu kuongoza Bunge hili maalumu na la kihistoria. Ushindi mkubwa mliopata ni kielelezo tosha cha imani kubwa na matumaini waliyonayo Wajumbe wenzenu kwenu. Matumaini yao ndiyo matumaini ya Watanzania wote, kwamba mtaliongoza vizuri Bunge hili, ili liweze kutimiza kwa ufanisi mkubwa jukumu lake muhimu sana katika historia ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Niruhusu pia niwapongeze kwa dhati Wajumbe wote wa Bunge Maalum la Katiba kwa bahati ya aina yake waliyopata ya kutunga Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Fursa hii hutokea mara chache sana katika historia ya nchi yo yote na watu wake. Mkifanikiwa kuipatia nchi yetu Katiba nzuri majina yenu yataandikwa kwa wino wa dhahabu, katika kumbukumbu za historia ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ni matarajio ya Watanzania kuwa mtatunga Katiba itakayokubalika na wengi. Katiba inayotekelezeka. Katiba itakayoimarisha Muungano wetu kwa kuondoa changamoto zilizopo sasa. Katiba itakayoipa nchi yetu mfumo bora wa kuongoza na kuendesha mambo yetu. Katiba itakayoimarisha umoja, upendo, ushirikiano na mshikamano miongoni mwa wananchi wa Tanzania, licha ya tofauti zao za asili za upande wa Muungano na maeneo watokako, au tofauti za jinsia, rangi, kabila, dini na ufuasi wa vyama vya siasa. Katiba itakayodumisha amani, usalama na utulivu nchini. Katiba itakayostawisha zaidi demokrasia, haki za binadamu, utawala wa sheria, utawala bora na kudhibiti maovu.
Na, mwisho ingawaje siyo mwisho kwa umuhimu, Katiba itakayoweka mazingira mazuri kwa uchumi wa nchi kukua, na wananchi wengi kunufaika sawia na maendeleo yatayopatikana.
Historia ya Katiba Nchini
Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wajumbe;
Hii itakuwa mara ya tatu tangu kuzaliwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Aprili 26, 1964, kwa nchi yetu kuwa na mchakato wa kutunga Katiba mpya. Mara ya kwanza ilikuwa mwaka 1965 ilipotungwa Katiba ya Muda na mara ya pili ni mwaka 1977 ilipotungwa Katiba ya Kudumu tuliyonao sasa. Tofauti na mara mbili zilizopita, safari hii mchakato unahusisha watu wengi zaidi. Wananchi wameshiriki moja kwa moja kutoa maoni yao kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, na ndio watakaofanya uamuzi wa mwisho kuhusu Katiba mpya kwa kura ya maoni. Wananchi pia walipata nafasi ya kuchagua Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya yaliyojadili Rasimu ya Kwanza ya Katiba. Pia walipata nafasi ya kutoa maoni yao kupitia Mabaraza ya Katiba ya taasisi. Katika Bunge hili wapo wananchi 201 kutoka makundi mbalimbali.
Katika mchakato wa kutunga Katiba za mwaka 1965 na 1977 kulikuwapo Tume za Kuandaa Rasimu na Bunge Maalum la Katiba kama ilivyo katika mchakato huu. Hata hivyo, kwa Katiba zilizopita Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano pekee ndio waliounda Bunge Maalum. Safari hii Bunge Maalum linajumuisha Wabunge, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na wananchi 201 wanaotoka kwenye jamii, wakiwakilisha asasi na makundi mbalimbali ya Watanzania kutoka Zanzibar na Tanzania Bara. Mchakato wa sasa utaishia kwenye kura ya maoni itakayoshirikisha wananchi wote wa Tanzania wanaoruhusiwa kupiga kura. Michakato iliyopita iliishia Bunge Maalum pekee.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Tangu kutungwa kwake, tarehe 25 Aprili, 1977, mpaka sasa Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977 imefanyiwa mabadiliko takriban mara 14. Mabadiliko hayo yalitokana na kufanyika au kutokea kwa mabadiliko muhimu ya kiuchumi, kisiasa na kijamii katika nyakati mbalimbali hapa nchini na katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Kwa ruksa yako naomba nitaje baadhi ya mabadiliko yaliyofanywa:-
Mabadiliko ya 1979 yaliunda Mahakama ya Rufani ya Tanzania kufuatia kufa kwa Mahakama ya Rufani ya Afrika Mashariki baada ya kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 1977.
Mabadiliko ya mwaka 1980 yalifanyika baada ya kutungwa kwa Katiba ya Zanzibar, hivyo kulazimu Katiba hiyo kutambulika kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano
Mabadiliko ya mwaka 1984 yaliweka utaratibu wa ukomo wa vipindi vya Urais ambao haukuwepo kabla ya hapo. Aidha, masuala ya Haki za Binadamu (Bill of Rights) yaliingizwa kwa mara ya kwanza katika Katiba. Vilevile, Mahakama ya Rufani ya Tanzania na mambo mengine ya iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki yaliongezwa katika Orodha ya Mambo ya Muungano.
Mwaka 1992, yalifanyika mabadiliko yaliyoanzisha Mfumo wa Vyama Vingi vya Siasa badala ya ule wa Chama kimoja uliokuwepo tangu 1965. Pia utaratibu wa uchaguzi wa Rais na Wabunge ulirekebishwa ili uendane na mfumo wa vyama vingi vya siasa. Vilevile utaratibu wa kuwa na viti maalum vya wanawake katika Bunge ulianzishwa. Wakati ule ilikuwa asilimia 15 ya Wabunge wote. Aidha, kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu Bunge lilipewa mamlaka ya kumwajibisha Rais na Waziri Mkuu kupitia kura ya kutokuwa na imani.
Mabadiliko ya mwaka 1994 yaliweka mfumo mpya wa kumpata Makamu wa Rais kupitia Mgombea Mwenza.
Mwaka 2000 na 2005, pamoja na mambo mengine yalifanyika mabadiliko yaliyopanua wigo wa Haki za Binadamu na kuongeza uwakilishi wa wanawake.
Umuhimu wa Mabadiliko ya Katiba
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kufanyika kwa mabadiliko hayo kunathibitisha utayari wa Serikali kufanya mabadiliko kila ilipoonekana inafaa kufanya hivyo. Pamoja na kufanya yote hayo na Serikali kuwa na msimamo huo, kumekuwepo na madai yaliyokuwa yanajirudia ya kutaka Katiba ya Tanzania iandikwe upya. Wako watu walioimithilisha Katiba yetu na nguo yenye viraka vingi mno kiasi kwamba ingefaa kununua mpya badala ya kuendelea kuivaa.
Madai ya kutaka Katiba mpya yalipazwa sauti baada ya kuanza kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa. Wapo waliokuwa wanadai Katiba mpya kwa imani, eti kwamba, itawawezesha kuishinda CCM. Lakini, si hayo tu, hata katika mchakato wa Serikali zetu mbili kushughulikia kero za Muungano, imedhihirika kuwa baadhi ya changamoto zilikuwa zinahitaji mabadiliko ya Katiba ili kuzipatia ufumbuzi wa uhakika na wa kudumu.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kwa kutambua ukweli huo na baada ya kushauriana na kukubaliana na viongozi wenzangu wakuu wa Chama tawala na Serikali zetu mbili wakati ule, ndipo tarehe 31 Desemba, 2010, nikatangaza dhamira ya kuanzisha mchakato wa kutunga Katiba mpya. Nilieleza siku ile kuwa katika mchakato huo tutakuwa na ushirikishwaji mpana wa wananchi wa Tanzania kwa makundi yao ya jinsia, dini, siasa na shughuli wazifanyazo kujipatia riziki na kwa maeneo wanayotoka katika pande zetu mbili za Muungano.
Mchakato wa Katiba Mpya
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Tarehe 16 Machi, 2011 Baraza la Mawaziri liliridhia kutungwa kwa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya kuliongoza taifa katika mchakato wa kutunga Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tarehe 18 Novemba, 2011 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. Kwa mujibu wa Sheria hiyo, mchakato wa kutunga Katiba Mpya ulikuwa unaanza kwa kuunda Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Tume hiyo imepewa jukumu la kusikiliza maoni ya wananchi mmoja mmoja na kwa makundi yao ya maslahi, taasisi zao na kupitia Mabaraza ya Katiba. Mwishowe Tume imetakiwa kutengeneza Rasimu ya Katiba mpya itakayofikishwa kwenye Bunge Maalum la Katiba kujadiliwa na Katiba mpya kutungwa. Mchakato wa Katiba utahitimishwa kwa wananchi kupiga kura ya maoni ya kuamua kama wanaikubali au kuikataa Katiba mpya.
Tarehe 6 Aprili, 2012 nilifanya uteuzi wa Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kuwaapisha tarehe 13 Aprili, 2012. Tume ilianza kazi tarehe 2 Mei, 2012 na kuikamilisha kwa mafanikio, hatua zote zilizoihusu na kukabidhi kwangu na kwa Rais wa Zanzibar, Taarifa ya Tume na Rasimu ya Katiba tarehe 30 Desemba, 2013. Kitendo cha Mwenyekiti wa Tume, Mheshimiwa Joseph Warioba kuwasilisha Rasimu hiyo mbele ya Bunge hili tukufu tarehe 18 Machi, 2014, kinahitimisha rasmi kazi ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Kazi inayofuatia ni ya Bunge hili kujadili, kuamua na kutunga Katiba mpya. Baada ya hapo Katiba mpya itafikishwa kwa wananchi kwa uamuzi wa mwisho kwa njia ya kupiga kura ya NDIYO au HAPANA.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Rasimu ya Katiba ilichapishwa kwenye gazeti la Serikali na magazeti mengine yanayosomwa na wananchi kama ilivyoagizwa katika Kifungu cha 20(2) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. Pamoja na hayo, Taarifa ya Tume na Rasimu ya Katiba viliwekwa wazi kwenye tovuti ya Tume kwa kila mtu kusoma. Inafurahisha kuona kuwa watu wengi wameisoma Taarifa ya Tume na Rasimu ya Katiba na kumekuwa na mjadala mpana kuhusu nyaraka zote hizo muhimu. Watu wengi wametoa maoni yao na wanaendelea kufanya hivyo. Kwa maoni yangu hili ni jambo jema sana na ni kielelezo thabiti kuwa demokrasia imestawi na inazidi kuota mizizi Tanzania. Pia, kwamba, Watanzania wako huru kushiriki na kutoa maoni yao kwa mambo yanayowahusu.
Pongezi kwa Tume
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kwa mara nyingine tena narudia kutoa pongezi za dhati kwa Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya uongozi wa Mheshimiwa Jaji Joseph Warioba akisaidiwa na Mheshimiwa Jaji Augustino Ramadhani, kwa kazi kubwa na nzuri waliyofanya. Kazi yao haikuwa rahisi hasa ukizingatia ukubwa wa nchi yetu, wingi wa watu wake, utitiri wa taasisi na pigo la kumpoteza Mjumbe mwenzao muhimu Dkt. Sengondo Mvungi aliyetangulia mbele ya haki katikati ya mchakato.
Pamoja na hayo, kwa bidii kubwa Wajumbe wa Tume wameweza kutembelea mikoa yote nchini na kuwafikia watu 351,644 waliotoa maoni yao kwa mdomo na kwa maandishi. Halikadhalika, walipokea na kuchambua maoni 772,211 kutoka kwa wananchi na taasisi mbalimbali. Baada ya kupokea maoni ya wananchi, kufanya utafiti na kwa kutumia maarifa na uzoefu wao, Wajumbe wakafanya kazi ngumu, kuliko yote, ya kutengeneza Rasimu ya Katiba iliyoko mbele ya Bunge hili. Ni kweli kwamba Wajumbe hawakuweza kuwafikia wananchi wote wa Tanzania, lakini wameweza kuwafikia wananchi wengi, ambao kwa kiasi kikubwa wanawakilisha taswira na mitazamo mipana ya jamii yetu.
Baadhi ya Masuala Yaliyojitokeza Katika Mjadala wa Mapendekezo ya Tume
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Tume imefanya kazi nzuri, yenye thamani kubwa na ya manufaa kwa taifa la Tanzania. Rasimu imeandikwa vizuri na kwa weledi wa hali juu. Tume imetoa mapendekezo ambayo kwa kiasi kikubwa yanahuisha na kuboresha Katiba ya nchi yetu, kwa namna ya pekee. Katiba inayopendekezwa, imejumuisha dhana na mambo kadhaa mapya yanayokwenda vyema na wakati tulionao na kuweka msingi mzuri kwa huko mbele tuendako. Kwa taratibu za kawaida za marekebisho ya Katiba tuliyonayo, isingekuwa rahisi kuingiza mambo mengi mapya kiasi hiki.
Wajumbe Wana Kazi Kubwa
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Waheshimiwa Wajumbe;
Rasimu ya Katiba ni kitabu kikubwa kilichosheheni mambo mengi. Kina kurasa 106, sura 17 na ibara 271. Wajumbe wa Bunge hili mnatakiwa kusoma na kuelewa vizuri kila kilichoandikwa ili muweze kufanya uamuzi ulio sahihi. Mnawajibika kuchambua kwa kina na umakini mkubwa kila kilichomo, sura kwa sura, ibara kwa ibara, sentensi kwa sentensi na hata neno kwa neno. Hamna budi kujiridhisha kuhusu uandishi wa vifungu vya Rasimu ya Katiba na kufaa kwa dhana mbalimbali zilizoingizwa na kujengeka katika Rasimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kile ambacho Wajumbe mtaona kinastahili kuboreshwa au kurekebishwa au kufutwa msisite kufanya hivyo ili Watanzania wapate Katiba iliyo bora. Msipofanya hivyo kuna hatari ya kupata Katiba ambayo ni ngumu kuitekeleza. Aidha, tunaweza kuwa na Katiba ambayo itanung'unikiwa na watu wengi na kusababisha madai ya kutaka ifanyiwe marekebisho muda mfupi baada ya kupitishwa. Bunge hili linao wajibu maalum wa kuzuia balaa hilo lisitokee katika nchi yetu. Ngazi mbalimbali zilizowekwa katika mchakato huu ni kama chujio la kuepusha hali hiyo isitokee. Kile ambacho hakikuonekana katika hatua moja kitaonekana katika hatua inayofuata na kurekebishwa. Nawaomba fursa mliyonayo muitumie vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Nimekwishaeleza kuwa moja ya jambo mnalotegemewa kufanya ninyi wenzetu mliopewa dhamana ya kutunga Katiba ya nchi yetu ni kujiridhisha na uandishi wake. Yapo maoni yaliyotolewa kuhusu uandishi ambayo naomba myatafakari na kuamua ipasavyo. Kwa mfano, kuna baadhi ya vifungu vya Katiba vinayopendekezwa vimekuwa na mambo mengi mno kuliko inavyostahili Katiba kuwa (too prescriptive). Pia kuna mawazo kwamba baadhi ya mambo hayangetakiwa kuwa katika Katiba bali yawe kwenye Sheria zinazotafsiri utekelezaji wa Katiba yenyewe.
Yako mambo yaliyotajwa kwenye Katiba ambayo yanatakiwa kuelezwa wazi kuwa mtu hatakwenda mahakamani kuidai Serikali impatie (non justiciable). Mambo yaliyotajwa kwenye Katiba ni mazuri na yanavutia, lakini lazima yaendane na uwezo wa nchi na uchumi wake kuhimili. Simaanishi kwamba tuyatoe kwenye Katiba, bali yabakie kama dhamira pale uwezo wa nchi utakaporuhusu yatekelezwe. Tusipofanya hivyo, kuna hatari ya Serikali kujikuta inalaumiwa au hata kufikishwa mahakamani kila wakati kwa madai ya jambo moja au jingine ambayo haina uwezo nayo. Ni muhimu sana mambo kama hayo muyatazame ili tusije kuwa na Katiba ambayo ni ngumu kutekeleza.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Yapo pia maoni kuwa baadhi ya vifungu vina upungufu katika uandishi wake, hivyo kuhitaji kufanyiwa marekebisho. Isipofanyika hivyo kunaweza kuwepo athari na nyingine zinaweza kuwa mbaya. Kwa mfano, Ibara ya 2 ya Rasimu inayotambulisha eneo na mipaka ya nchi yetu. Ibara hiyo inasomeka kuwa "Eneo la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni eneo lote la Tanganyika likijumuisha sehemu yake ya bahari na eneo lote la Zanzibar likijumuisha sehemu yake ya bahari".
Maelezo hayo yameacha kutambua, kwa upande wa Tanzania Bara, sehemu yetu ya maziwa na mito ambayo ni kubwa sana. Kwa nini tuache kuitaja? Je hatutoi nafasi kwa nchi tunazopakana nazo siku moja wakaja kupora sehemu zetu hizo na sisi kukosa utetezi kwa kuwa hata Katiba yetu haikuyatambua maeneo hayo kuwa ni yetu? Hili ni jambo kubwa ambalo Bunge hili lazima mlirekebishe. Wakati ndiyo huu hakuna mwingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Jambo jingine kuhusu uandishi ni mgongano kati ya pendekezo la msingi la Tume la kuwa na muundo wa Serikali tatu na majukumu ya Serikali ya Muungano ambayo kimsingi ni majukumu ya Serikali za nchi washirika. Katika Rasimu hii malengo ya taifa yameainishwa na Serikali ya Muungano inatakiwa kuhakikisha kuwa malengo hayo yanatekelezwa na itoe taarifa Bungeni. Katika mfumo wa Serikali tatu unaopendekezwa na Tume masuala yahusuyo uchumi na maendeleo ya jamii kama vile kukuza kilimo, ufugaji, uvuvi, viwanda, biashara, pembejeo, elimu, hifadhi ya jamii na kadhalika yako chini ya mamlaka ya Serikali za nchi washirika. Mamlaka ya Serikali ya Muungano ni kwa mambo saba tu yafuatayo:- Katiba na Mamlaka ya Jamhuri ya Muungano, Ulinzi na Usalama wa Jamhuri ya Muungano, Uraia na Uhamiaji, Sarafu na Benki Kuu, Mambo ya Nje, Usajili wa Vyama vya Siasa, Ushuru wa Bidhaa na Mapato yasiyo ya kodi yatokanayo na Mambo ya Muungano.
Kwa Rasimu kupendekeza muundo wa Serikali tatu na kuipa Serikali ya Muungano majukumu ambayo haina mamlaka nayo, ni kuzusha utata na migongano kati ya Serikali ya Muungano na nchi washirika. Mkichagua mfumo wa Serikali tatu, inawalazimu muyaondoe mambo hayo kwani Serikali ya Muungano haistahili kuyatekeleza na wala haina uwezo wa kuweka masharti kwa Serikali za nchi washirika kwa mambo yaliyo kwenye mamlaka ya nchi hizo. Lakini kama mtaamua tuendelee na muundo wa Serikali mbili, mambo haya mazuri yanatekelezeka na Serikali ya Muungano bila ya matatizo. Katika uandishi wa Rasimu Utumishi katika Serikali ya Muungano haumo katika Orodha ya Mambo ya Muungano. Ni lazima liwemo. Hayo ni baadhi tu ya masuala yahusuyo uandishi katika Rasimu. Naamini mkiisoma Rasimu kwa makini mnaweza kuyagundua mengineyo.
Dhana Mpya
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Katika Rasimu kuna dhana mpya na mambo mapya kadhaa yaliyoingizwa ambayo yanabadili utaratibu wa sasa wa uendeshaji wa nchi na mambo mbalimbali. Nawaomba mfanye uchambuzi wa kina kwa kila kinachopendekezwa na kujiridhisha kuhusu kufaa kwake na manufaa yake. Fanyeni hivyo ili tujihakikishie kuwepo kwa mambo mazuri na uendeshaji mzuri wa shughuli katika taifa letu changa.
Mambo ni mengi na kwa ufinyu wa muda sitaweza kuyazungumzia yote. Niruhusuni nizungumzie baadhi ya dhana na mambo mapya yaliyomo katika Rasimu. Jambo la kwanza, kwa mfano, linahusu Ibara ya 128 (2)(d) inayoleta dhana ya "Mbunge kupoteza Ubunge iwapo atashindwa kufanya kazi za Mbunge kwa miezi sita mfululizo kutokana na maradhi au kizuizi ndani ya gereza".
Watu hawana tatizo na Mbunge kuwa kizuizini ndani ya gereza kama amepatikana na hatia Mahakamani na kuhukumiwa kifungo. Lakini, isijekuwa yuko rumande kwa tuhuma akisubiri kesi kusikilizwa. Je akija kuonekana hana hatia na kuachiliwa? Naungana na wale wanaoshauri kuwa jambo hili lifafanuliwe vizuri na kutambua Mbunge kutiwa hatiani na kupata adhabu ya kifungo cha kipindi hicho. Ni bora ifanyike hivyo sasa ili kuondoa mikanganyiko. Hakuna haja ya kusubiri mpaka jambo hili lije kufafanuliwa baadaye kwa Sheria itakayotungwa na Bunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Kwa upande wa mtu kupoteza Ubunge kwa sababu ya "kuugua kwa miezi sita mfululizo" ni maoni ya watu wengi kuwa huu ni ukatili ambao haustahili kufanywa na Katiba. Kuugua ndiyo ubinadamu na wakati mwingine Mbunge anaweza kupata ajali akiwatumikia wananchi wa Jimbo lake. Anaweza kuugua kwa miezi sita au zaidi na kupona kabla ya kipindi chake cha Ubunge kufika mwisho. Kwa nini awekewe ukomo wa miezi sita? Katiba ya mwaka 1977 tunayotumia sasa haina sharti hilo. Watu wanauliza hoja na haja ya kuwa na sharti hili kwenye Katiba mpya ni ipi? Wanasema kwa kweli anachostahili Mbunge huyu kufanyiwa ni kuuguzwa afya yake iimarike ili aendelee kutumikia watu wake, na siyo kupoteza uongozi wake. Tusiwatie watu kishawishi cha kukatiza matibabu ili kukwepa sharti hilo. Ni vyema jambo hili mkalitazama kwa makini, na muone kama linastahili kuwepo au hapana.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Katika Rasimu hii imeingizwa dhana mpya ya kuweka ukomo wa vipindi vitatu kwa Wabunge. Tena mapendekezo haya hayasemi vipindi vitatu mfululizo au la!. Jambo hilo limezua mjadala motomoto katika jamii. Ni vizuri mkajiridhisha juu ya sababu za msingi na manufaa ya kufanya hivyo hapa Tanzania. Mazoea yetu na ya kwingineko duniani ni kuweka ukomo kwa Wakuu wa Nchi kwa sababu nzuri na rahisi kuzielezea. Lakini, kuwawekea ukomo Wabunge ni jambo jipya na huenda Tanzania tukawa wa kwanza. Nashawishika kuungana na wale wanaopendekeza kuwa pengine ni mapema mno kuanzisha utaratibu huo hapa kwetu.
Nachelea kuwa tutainyima nchi yetu fursa ya kupata watu wenye maarifa na uzoefu mzuri wa uongozi kwa nafasi ya Ubunge au kwa nafasi za uongozi wa Taifa bila ya sababu za msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Jambo lingine jipya linalopendekezwa na Tume ni utaratibu wa kumuondoa Mbunge katikati ya kipindi chake cha uongozi. Kwa hoja linaonekana kuwa jambo jema lakini naomba athari zake mzitafakari vizuri. Kuna hatari ya kuanzisha misuguano kwenye Majimbo na kuwaacha Wabunge wasifanye kazi zao kwa utulivu bali wawe wanajihami dhidi ya wapinzani wao kuwatengenezea fitna za kuwatoa. Utaratibu unaopendekezwa wa Chama chake kujaza nafasi ya Mbunge inapokuwa wazi katika mazingira hayo nao unaweza kuwa ndicho kichocheo kikubwa cha vuguvugu la kumuondoa Mbunge. Walioshindwa kwenye kura ya maoni wanaweza kufanya kazi ya kuwachimba wenzao mpaka waondoke. Jipeni muda wa kupima faida na hasa thamani inayoongezwa na kuanzisha utaratibu huo. Naomba tujiridhishe kama jambo hili jipya lina tija. Hivi kupewa nafasi kila miaka mitano kurudi kwa wananchi hakutoshi kumuondoa Mbunge ambaye watu wamemchoka?
Muundo wa Muungano
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Jambo lingine kubwa lililopendekezwa na Tume ambalo limevuta hisia za karibu watu wote nchini linahusu muundo wa Muungano wetu kuwa wa Serikali tatu badala ya mbili za sasa. Pendekezo hili limezua mjadala mkubwa tangu lilipotolewa katika Rasimu ya kwanza na kurudiwa katika Rasimu ya pili. Wakati mwingine mjadala umekuwa mkali na wa hisia kali kwa kila upande.
Kwa kweli hili ndilo jambo kubwa kuliko yote katika Rasimu kwa sababu linapendekeza kuanzishwa kwa muundo na mfumo mpya wa kuendesha nchi yetu. Hii ndiyo agenda mama ya Bunge hili ambayo kila Mtanzania anasubiri kwa hamu uamuzi wenu utakuwa upi. Ombi langu kwenu ni kuwa watulivu mnapojadili suala hili. Epukeni jazba ili mfanye uamuzi ulio sahihi. Lazima mtambue uamuzi usiokuwa sahihi kwa jambo hili una hasara kubwa. Tunaweza kupoteza kitu tulichokijenga kwa gharama kubwa kwa nusu karne iliyopita. Tanzania inaweza kuwa nchi iliyojaa migogoro na matatizo mengi ambayo hatunayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wajumbe;
Kama alivyoeleza Mwenyekiti wa Tume Mheshimiwa Jaji Joseph Sinde Warioba, mara kadhaa, mjadala au madai ya kutaka muundo wa Serikali tatu si jambo jipya. Ulikuwepo hata wakati wa mazungumzo ya kuunganisha nchi zetu mbili mwaka 1964. Ulikuwa kiini cha kuchafuka kwa hali ya hewa ya kisiasa Zanzibar mwaka 1984. Muundo huu uliwahi kupendekezwa na Tume ya Nyalali mwaka 1992, ndiyo hoja ya G55 mwaka 1993 na umependekezwa pia na Tume ya Jaji Kisanga ya mwaka 1998. Lakini mara zote hizo mapendekezo hayo hayakukubaliwa.
Waasisi wa taifa letu, yaani Mwalimu Julius Nyerere, aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Tanganyika wakati ule na Sheikh Abeid Amani Karume, aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar wakati ule, waliamua kuchagua Muungano wa Serikali mbili tulionao sasa. Walitoa sababu mbili kuu: "ni muundo unaoihakikishia Zanzibar kuwa haimezwi na Tanganyika; na pia unaiepusha Tanganyika kubeba mzigo mkubwa wa kugharamia Serikali ya Tanganyika na ile ya Muungano".
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Natambua kuwepo kwa rai ya kutaka Mwalimu Nyerere asitumiwe katika mjadala huu. Nionavyo mimi ni vigumu kuacha kujadili fikra za Mwalimu Nyerere na Sheikh Karume katika jambo hili. Wao ndiyo wa mwanzo kujadili na kukubaliana kuwa mfumo wa Serikali mbili ndiyo bora kwa nchi yetu. Iweje leo tunapozungumzia kuubadili, mawazo yao yawe hayafai kutumika au hata kuzungumzwa. Hivi hasa mawazo ya nani pekee ndiyo bora zaidi kutumika? Tutakuwa hatuutendei haki mjadala huu na sisi wenyewe tunaoshiriki katika mchakato huu. Rai yangu kwenu ni kuwa mzitazame hoja zote kwa marefu na mapana yake ili mpime kama zipo sababu za kuubadili muundo wa sasa wa Muungano wa Serikali mbili na kuleta wa Serikali tatu. Na, kama zipo mabadiliko hayo yaweje! Lazima mfanye uamuzi kwa utambuzi na hoja zenye mashiko. (you must make an informed decision).
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Tume imetoa sababu mbili kubwa za kupendekeza muundo wa Serikali tatu. Sababu ya kwanza ni kwamba ndiyo matakwa ya Watanzania wengi kote Zanzibar na Tanzania Bara. Inaeleza kuwa idadi kubwa ya Watanzania waliotoa maoni, yaani asilimia 60.2 wa kutoka Zanzibar wanaunga mkono muundo wa Serikali ya Mkataba, na asilimia 61.3 wa kutoka Tanzania Bara wanaunga mkono muundo wa Serikali tatu. Sababu ya pili ni kwamba muundo huo unatoa majawabu ya uhakika na endelevu kwa changamoto za muundo wa sasa wa Serikali mbili zinazonung'unikiwa na watu wa pande zetu mbili za Muungano.
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Sababu hizi mbili kuu zilizotolewa na Tume zimezua mjadala mkali katika jamii. Wapo wanaokubaliana na Tume na wapo wasiokubaliana nayo. Wapo wanaosema Tume imesema kweli kwamba Watanzania wengi wanaunga mkono muundo wa Serikali tatu, hivyo muundo wa Serikali tatu hauepukiki. Ndiyo matakwa ya wengi hivyo msemo wa Kiswahili usemao wengi wape uheshimiwe.
Lakini wapo wanaodai kuwa takwimu za Tume hazionyeshi ukweli huo. Wanasema kuwa taarifa ya Tume imeonesha kuwa Watanzania waliotoa maoni yao kwa Tume kwa mdomo na maandishi walikuwa 351,664. Kati yao ni wananchi 47,820 au sawa na asilimia 13.6 ndiyo waliokerwa na muundo wa Muungano hivyo wakauzungumzia. Wananchi 303,844 au sawa na asilimia 86.4 muundo wa Muungano kwao halikuwa tatizo, ndiyo maana hawakuuzungumzia kabisa. Wanahoji kuwa iweje leo asilimia 13.6 ya Watanzania wote waliotoa maoni wageuke kuwa ndiyo Watanzania walio wengi!
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Wanasema pia, kwamba mbona Taarifa ya Tume yenyewe, kuhusu takwimu (uk. 66 na 67), inaonesha kwamba kati ya hao watu 47,820 waliotoa maoni kuhusu Muungano, ni watu 17,280 tu ambao ni sawa na asilimia 37.2 ndiyo waliotaka muundo wa Serikali tatu, asilimia 29.8 walitaka Serikali mbili, asilimia 25.3 walipendekeza Serikali ya Mkataba na asilimia 7.7 walipendekeza Serikali moja. Hii hoja ya Watanzania wengi kutaka Serikali tatu msingi wake upi?
Mheshimiwa Mwenyekiti;
Takwimu za Tume (uk. 57) zinaonyesha, vilevile kuwa Tume ilipokea maoni 772,211. Kati ya hayo asilimia 10.4 tu ndiyo yaliyozungumzia muundo wa Muungano na asilimia 88.6 hayakuzungumzia Muungano bali mambo mengine. Hivyo basi wanahoji pia kwamba kama muundo wa Muungano ungekuwa ni jambo linalowakera Watanzania wengi, lingedhihirika kwenye idadi ya watu waliotoa maoni na kwenye idadi ya maoni yaliyotolewa. Yote hayo hayakujitokeza. Waliouzungumzia Muungano walikuwa asilimia 13.6 tu ya watu wote waliotoa maoni na maoni yanayohusu Muungano yalikuwa asilimia 10.4 ya maoni yote. Hivyo basi, wanauliza "usahihi wa hoja ya Watanzania wengi kutaka Serikali tatu uko wapi?"
Changamoto za Muundo wa Serikali Mbili
Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wajumbe;
Kama nilivyokwishagusia awali, sababu ya pili ambayo Tume inatoa kuhusu kufaa kwa muundo wa Serikali tatu ni kwamba mfumo huu unajibu changamoto nyingi za muundo wa Serikali mbili. Tume imeainisha vizuri changamoto za muundo wa Serikali mbili. Kwa upande wa Zanzibar wanalalamikia kile kinachoitwa Tanzania Bara kuvaa koti la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na hivyo kutumia mamlaka ya Serikali ya Muungano kujinufaisha yenyewe. Fursa hiyo Zanzibar hainayo. Aidha, wanasema mipaka na mamlaka ya Serikali ya Muungano kwa mambo ya Muungano, na kwa mambo ya Tanzania Bara haijaainishwa vizuri ikaeleweka. Wazanzibari pia, wanazungumzia mkanganyiko kuhusu ugawanaji wa mapato, na jinsi ya kuchangia shughuli za Muungano baina ya Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Vilevile, wanalalamikia Rais wa Zanzibar kuondolewa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano.
Aidha, kuna malalamiko kuwa orodha ya mambo ya Muungan
Share:

0 maoni:

MATUKIO YA VIDEO

Kumbukumbu la Blogu

Recent Posts

Unordered List

Pages

Theme Support

Sample Text