
Dk. Slaa, alitoa kauli hiyo juzi usiku jijini Mwanza katika kipindi cha ‘Ajenda 2015’, kinachorushwa moja kwa moja na kituo cha televisheni cha Star Tv.
Kiongozi huyo alikuwa akijibu swali la mtangazaji wa kipindi hicho, Dotto Bulendu, aliyetaka kujua ni kwanini Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) wameamua kuanza ziara mikoani kuwaelimisha wananchi wakati mchakato wa katiba ndio upo katika hatua ya rasimu ya pili kujadiliwa bungeni.
“Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete alipoenda kuzindua Bunge, alitumia muda huo kutoa semina elekezi na kutangaza msimamo wa Chama Cha Mapinduzi ambao haukujali maoni ya wananchi,” alisema Dk. Slaa.
Alisema Watanzania wanapaswa kuelewa kuwa CHADEMA walipokuwa wanapigania sheria ya mabadiliko ya katiba kutaka rais asiwe na mamlaka makubwa katika kuteua wajumbe wa Bunge Maalumu, walibaini athari za mchakato kutekwa na chama tawala.
Alibainisha kuwa msemaji wa kambi rasmi ya upinzani kuhusu mambo ya katiba na sheria, Tundu Lissu, aliyekuwa akipinga jambo hilo, alionekana ni mbishi, asiyependa kuwasikiliza wengine, lakini athari ya uteuzi inaonekana sasa.
Dk. Slaa, alisema wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba asilimia kubwa ni wanachama wa CCM kwa kivuli cha kupitia kwenye asasi mbalimbali.
Alisema vyama vinavyounda Ukawa, vimeamua kwenda kwa wananchi nchi nzima kuwaeleza ukiukwaji wa kanuni uliofanywa kwa makusudi na Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, Samuel Sitta, ambaye aliruhusu Jaji Warioba awasilishe rasimu kabla ya hotuba ya ufunguzi ya Rais Kikwete.
Alibainisha kuwa kilichofanywa na Sitta kililenga kutoa fursa kwa Rais Kikwete kuwachanganya wananchi kwa kupinga maoni ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba aliyoiunda.
Dk. Slaa, aliongeza kuwa Ukawa wamejitokeza sasa kutokana na serikali kutumia nguvu nyingi ikiwemo vyombo vya habari kuchakachua maoni ya wananchi.
“Tume ni ya rais mwenyewe, ilitumwa kukusanya maoni na yeye mwenyewe, hadidu za rejea alitoa yeye, na ushahidi upo amefanya mahojiano ya mara kwa mara na tume, hivyo kuja kukataa maoni ya wananchi, ni dharau na matusi kwa Watanzania waliotoa maoni,” aliongeza Dk. Slaa.
Dk. Slaa, alikemea matamko yanayotolewa na baadhi ya watu kukataa kuheshimu maoni ya wananchi, akitolea mfano kauli ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana aliyoitoa wiki iliyopita katika viwanja vya Mwembeyanga, Temeke jijini Dar es Salaam.
Akihutubia mkutano wa wanachama wa CCM, Kinana alikaririwa akisema; “mchakato wa katiba mpya unaoendelea bungeni mjini Dodoma, msimamo wa CCM utaendelea kuwa ni serikali mbili.”
Alisema hotuba iliyotolewa na Rais Kikwete, wakati akizindua Bunge la Katiba, imetoa mwelekeo mpya kwa wajumbe wa Bunge.
Mchangiaji mwingine katika kipindi hicho aliyejulikana kama Solomon Lufunda aliyekuwa katika kipindi hicho upande wa Dar es Salaam, alisema kuwa mchakato wa katiba umeingiliwa zaidi na serikali na kuwanyima wananchi fursa.
Lufunda alisema kuwa CCM imeingilia na inavuruga mchakato wa katiba, haiheshimu matakwa ya wananachi.
Alikemea vikali kauli ya hofu iliyosemwa na Rais Kikwete kuwa endapo wananchi wataunga mkono serikali tatu, basi jeshi litapindua serikali na kuongoza nchi, au kuleta machafuko nchini.
Mara baada ya uteuzi wa wajumbe wa Bunge la Maalumu la Katiba, Mbunge wa Singida Mashariki ambaye ndiye msemaji katika suala la katiba na sheria, Lissu, alinukuliwa akisema:
“Sisi CHADEMA tulisema tangu mwanzo kuwa tukimuachia Rais Jakaya Kikwete afanye uteuzi ni kuhalalisha kupata katiba ya ubabaishaji, na hili linaashiria kutokea baada ya wajumbe wa CCM kuwa wengi kuliko vyama vingine.”
Alisema wajumbe walioteuliwa wanaonyesha namna gani wanavyorudisha asante kwa Rais Kikwete kutokana na kuteuliwa katika nafasi hiyo, dalili inayoonyesha kuwa wajumbe hao ni watu wake na wataenda kutekeleza masilahi yake badala ya wananchi.
Lissu alisema licha ya wajumbe wengi kuonyesha wazi kuwa na masilahi na Rais Kikwete, CHADEMA itapambana kuhakikisha kuwa katiba inayopatikana inakuwa kwa masilahi ya wananchi na si wanasiasa.
(J.G)
0 maoni:
Chapisha Maoni