Jumatano, 2 Aprili 2014

Waziri asisitiza utunzaji wa vyanzo vya maji nchini


Profesa_Maghembe_Waziri_wa_Maji_51c73.png
Na Joel Mangoma
SERIKALI imesisitiza umuhimu wa utunzaji wa vyanzo vya maji kwa faida ya ustawi wa wananchi na maendeleo ya uchumi wa taifa kwa ujumla.
Kauli hiyo ilitolewa hivi karibuni mjini hapa na Waziri wa Maji Profesa Jumanne Maghembe, alipokuwa akiweka jiwe la msingi kwa ajili ya mradi wa upanuzi wa mtandao wa maji ya Ziwa Victoria kutoka Kijiji cha Mhalo hadi mji wa Ngudu wilayani Kwimba.
Alisema lazima wananchi kutunza vyanzo vya maji ili kuepuka ukame unaoweza kutokea kutokana na uharibifu huo wa mazingira, na kwamba serikali inajitahidi kuhakikisha vyanzo vya maji vinalindwa ili kuepuka ukame.
"Tungependa wananchi wafahamu kuwa kutunza vyanzo vya maji ni kwa faida yao wenyewe, kwa vizazi vya sasa na vijavyo... kwa kufanya hivyo watajiwekea mazingira mazuri ya kujenga uchumi wa nchi.
"Rasilimali za maji zinapungua kwa kasi, hii yote ni kutokana na uharibifu wa mazingira," alisema Profesa Maghembe huku akitoa mifano ya maeneo kati ya mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro na Dodoma iliyokumbwa na uhaba wa maji.
Alisema wakati wa kiangazi maji yanakauka kwenye baadhi ya mito nchini jambo linaloleta hatari kwa afya ya binadamu na maisha ya viumbe majini na nchi kavu.
Akitoa mifano zaidi ya mito ambayo ilikuwa na maji na sasa imekauka, alisema maji yanayopita Dumila katika Mto Wami ni kidogo wakati kipindi cha nyuma maji yalikuwa yanapatikana kipindi chote cha mwaka bila kukauka.
"Ukipanda kwenye milima ya Usambara toka Korogwe hadi Bwiko utaona mito yote imekauka, mto pekee uliobaki ni ule wa Mkomazi, hii ni hatari," alisema waziri huyo.
Alielezea tatizo la mabadiliko ya tabia nchi husababisha upungufu wa maji katika maeneo mengi na kuwa maeneo yaliyokuwa yanapata milimita 1,000 kwa mwaka sasa hivi yanapata milimita 500.
Share:

0 maoni:

MATUKIO YA VIDEO

Recent Posts

Unordered List

Pages

Theme Support

Sample Text